The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Mhe. Balozi na Waheshimiwa Mabalozi Wateule ‘Tanzania ni sehemu sahihi ya kuwekeza’ .


4 Novemba,2019: Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetembelewa na anayekwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait Mhe. Balozi Inj. Aisha Amour na Waheshimiwa Mabalozi Wateule tisa  ambao hivi karibuni waliteuliwa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwakilisha nchi nje ya nchi. Waheshimiwa hao wamefika na kupokelewa  na timu ya TIC ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mafutah Bunini kwa lengo la kuongezewa uelewa wa masuala ya uwekezaji wanapokuwa wakielekea kutekeleza na kusimamia masuala ya Diplomasia (Uwekezaji, Biashara na Utalii) nje ya nchi. 

 

Kipekee kabisa  Bw. John Mnali, Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji amewaeleza Waheshimiwa hao  taarifa za fursa za uwekezaji zinazonadiwa kwa sasa, mbinu za kuvutia uwekezaji, changamoto za uwekezaji  na miongozo stahiki ya namna ya kushawishi na kuvutia wawekezaji nchini katika hatua za awali. Sambamba na hayo pia Waheshimiwa wamepata nafasi ya  kupata uelewa juu ya taarifa muhimu za awali anazopaswa kuambiwa mwekezaji, huduma atakazopata mwekezaji katika kufanikisha uwekezaji wake nchini kupitia Mfumo wa Huduma za Mahala Pamoja, vivutio vya uwekezaji, na maboresho mbalimbali yanayochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara kiujumla.  Aidha Bw. Mnali pia amebainisha maeneo ambayo Mabalozi watahitajika kushirikiana na TIC hususan kuandaa makongamano ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kunadi fursa za uwekezaji, kuvutia  wawekezaji wapya, mitaji, tekinolojia, ujuzi na miradi ya ubia.

 

Kwa upande wao Waheshimiwa, wameshukuru kwa elimu ya masuala ya uwekezaji kutoka TIC na kwamba imewapa mwongozo zaidi kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao yatakayohusiana na uwekezaji. Wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na TIC ili kufanikisha uwekezaji wa wawekezaji watakaoonesha nia ya kuwekeza Tanzania kutoka nchi wanazoziwakilisha.

 

Naye Bw. Bunini amehitimisha kwa kuwatakia heri Waheshimiwa katika vituo vyao vya kazi watakavyopangiwa na kuwataka kwa pamoja tuinadi ‘Tanzania kuwa ni sehemu sahihi ya kuwekeza’. Uongozi wa TIC upo tayari  kufanya kazi na  ofisi za balozi zetu nje ya nchi katika kufanikisha uwekezaji zaidi muda wote.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)