The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Injinia Evarist Ndikilo amekipongeza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwa taasisi wezeshi wa uwekezaji kivitendo .


27Agosti, 2019:  Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Injinia Evarist Ndikilo amekipongeza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwa taasisi wezeshi wa uwekezaji kivitendo.Hii ni kutokana na namna ambavyo wanaongoza na kusaidia wawekezaji kufahamu hatua zote za msingi za kuanzisha miradi/kuwekeza nchini sambamba na kuwasaidia kupata vyeti, leseni na vyeti muhimu vya uwekezaji. Huduma hizo kutoka taasisi na mamlaka mbalimbali zinapatikana ndani ya ofisi ya TIC kupitia Mfumo wa Mahala Pamoja. Mhe. Ndikilo ameyazungumza hayo Rufiji alipokuwa kwenye sherehe za uwekwaji wa jiwe la msingi kwenye kiwanda cha kampuni ya Huatang, cha kutengeneza lead ingot kutokana na betri chakavu/ zilizokwisha muda wake za magari na pikipiki. Bidhaa hiyo itakayozalishwa kwa sasa itakuwa ikisafirishwa nje ya nchi kama malighafi ya kutengeneza betri mpya za magari na pikipiki mpaka hapo kampuni itakapoanza uzalishaji wa betri mpya nchini.

 

"Nawashukuru sana TIC kuwaongoza ndugu zetu hawa katika hatua zote za kuwekeza na hatimaye wamefanikiwa kuanzisha uwekezaji wao Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Hii kwetu ni neema, na Rufiji inaenda kuwa juu. Hatua hii imefikiwa kutokana na juhudi za Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli kushughulikia changamoto za Wilaya ya Rufiji ikiwamo kuweka miundombinu wezeshi hususan. Na wananchi watarajie viwanda vingi kutokana na mategemeo ya umeme wa uhakika unaotarajiwa kuzalishwa kutoka Bwawa la Nyerere, uwepo wa maeneo ya viwandac "Alisema Mhe. Ndikilo.

 

Akiendelea na hotuba yake, Mhe. Ndikilo ameipongeza kampuni ya Huatan kupitia Mkurugenzi wake   Bw. Ding Xuan kwa kuthubutu na kuamua kuanzisha kiwanda hicho Wilayani Rufiji. Mkoa una matumaini kwamba kiwanda kitakuwa chachu ya kuwavuta wawekezaji wengine pamoja na kuleta ajira, maendeleo usafi wa mazingira, soko, fursa kwa wakazi wa Rufiji na Taifa kwa ujumla. Pamoja na hayo Mhe. Evarist amewataka wananchi wa Nyamwage kuupokea mradi huo na kushirikiana na mwekezaji vizuri ili kupitia mafanikio ya mradi wao akawe balozi mzuri wa kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wengine tena kwa wingi Wilayani Rufiji. Jambo hili ni wazi kwamba Huatang ni miongoni mwa viwanda vichache katika Wilaya ya Rufiji ingawa kuna uwekezaji mwingi na mkubwa katika Mkoa wa Pwani ukilinganisha na  Wilaya ya Kisarawe,  Mkurunga na Pwani.

 

"Niwaombe Wananchi wa Nyamwage, kushirikiana vizuri na Wawekezaji wetu wa kiwanda hiki. Ushirikiano ni Muhimu sababu hawa ndio mabalozi huko kwao kwamba sasa Rufiji inafaa kwa uwekezaji wa viwanda" Amesema Mhe. Evarist.

 

Kwa upande wa TIC, katika sherehe hizo Meneja wa Kanda ya Mashariki Venance Mashiba, amekiwakilisha Kituo. Na akiongea na vyombo vya habari Mashiba amesema  kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo  ni hatua kubwa  kwa TIC na mradi huo ulisajiliwa Novemba, 2017. Aidha amesema, mradi huo wenye thamani ya dola za kimarekani zaidi ya laki sita 600,000 uchukuliwe na watanzania kama fursa ya ajira na unategemewa kukamilika ifikapo Machi, 2020. 

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kkampuni hiyo Bw. Ding Xian amesema ameanzisha mradi huo ikiwa ni kuitikia wito wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Balozi wa China ambao wanawahamisha Wachina kuanzisha viwanda Tanzania kutokana na kuwapo kwa mazingira mazuri. Bw Ding ameomba ushirikiano wa wadau wote katika kufanikisha uwekezaji huo Wilayani Rufiji kwa maslahi ya nchi zote (Tanzania na China).

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)