The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Mabalozi wameaswa kuendelea kuunga juhudi za Serikali kwa kutafuta wawekezaji watakaowekeza kwenye miradi yenye kuleta manufaa ya nchi kutoka nchi wanazowakilisha .


Agosti, 2019: Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Geoffrey Mwambe ametoa mada kwa Mabalozi takriban arobaini  na tatu (43) wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani. Mabalozi hao wamekutana kwa pamoja kupitia kikao kazi kilichosimamiwa na Mwenyekiti wa Mbalozi hao Mhe. Prof. Paramagamba Kabudi kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa diplomasia ya uchumi katika nchi ambazo Waheshimiwa Mabalozi wanaziwakilisha.

 

Akizungumza na vyombo vya habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Paramagamba  amesema, Mabalozi hao kwa uwingi wao wamefika nchini kwa pamoja likiwa ni jambo la kawaida wakati wa mikutano ya SADC ambapo Mabalozi wote wa nchi ambayo inapokea Uenyekiti wanatakiwa kurejea nchini. Hii ni Kutokana na taratibu kwamba Mabalozi wa  nchi ambayo Rais wake amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC pia kwa kipindi husika katika nchi wanazoziwakilisha, wanakuwa Wenyeviti wa Mabalozi wa nchi za SADC. Kufuatia utaratibu huo, Waheshimiwa Mabalozi walirejea nchini ili kupewa maelekezo na miongozo ya kufanikisha majukumu hayo yatakayoendana sambamba na uwakilishi wao nje ya nchi.  Aidha Mhe. Kabudi pia alieleza  kwamba,  Mabalozi hao wamerejea nchini kufuatia utaratibu za nchi yetu ambapo baada ya muda, Mabalozi huitwa ili kuja kuona na kutembelea miradi ya kimkakati inavyotekelezwa na Serikali na kujifunza namna inavyoakisi hatua ya maendeleo iliyofikiwa. Ziara hiyo pia huwasaida  kuona  fursa za uwekezaji, biashara na utalii, kupata mafunzo ya umuhimu na faida za uwekezaji  na kupewa elimu ya namna bora ya kuhamsisha na kuvutia uwekezaji kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa muktadha huo, Waheshimiwa Mabalozi wamepata nafasi ya kusikiliza mada kutoka Taasisi za Serikali Tanzania Bara na Visiwani ambapo TIC pia imekuwa miongoni mwa taasisi zilizotoa mada.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Mwambe katika kuanza  mada yake alisema  kuwa, kuna mahusiano ya moja kwa moja ya ufanyaji kazi kati ya TIC na Ofisi za Balozi zetu nje ya nchi. Hii ni kutokana na sababu kubwa kwamba unapozungumzia diplomasia ya kiuchumi  inayotekelezwa na Mabalozi maana yake unalenga mambo makuu matatu ambayo ni biashara, uwekezaji na utalii. Hivyo mada ya Mwambe kuhusu TIC kama mratibu mkuu wa masuala ya uwekezaji nchini, alifafanua zaidi uwepo wa  mazingira mazuri  ya uwekezaji kutokana na mikakati endelevu ya maboresho inayotekelezwa na Serikali, fursa za uwekezaji, umuhimu wa kuvutia uwekezaji/kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi yetu, sababu za kuwekeza Tanzania(masoko na rasilimali) , namna ya kuwahudumia wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza nchini na   changamoto zilizopo ili kuchangia katika kuzitafutia ufumbuzi . Lengo ni kufanikisha mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Mhe.. Dkt. John Pombe Magufuli kuifikia Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati ifikapo 2025.

 

Aidha, Mwambe amewashukuru Waheshimiwa Mabalozi kwa ushirikiano wanaoipatia TIC katika kufanikisha masuala ya uwekezaji nchini (kuandaa makongamano ya uwekezaji ya ndani na nje ya nchi) na amewaomba waendelee kushirikiana katika kuvutia mitaji ya uwekezaji kutoka nje (FDI) ambacho ni kiungo muhimu kukuza uchumi wa nchi. Amehitimisha kwa kuwahakikishia  Waheshimiwa Mabalozi utayari wa Kituo kuendeleza mashirikiano yaliyopo  ili kufanikisha utafutaji wa wawekezaji watakaowekeza kwenye miradi yenye kuleta manufaa ya nchi. Miradi hiyo ni ile itakayolenga kwenye sekta za uongezaji thamani mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji, viwanda, uzalishaji wa sukari, mafuta ya kula, madawa na vifaa tiba, uunganishaji wa magari, uongezaji thamani madini na utengenezaji wa madawa na vifaa tiba na utalii.

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)