The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Rais wa Tanzania na Afrika Kusini kwa pamoja wameshiriki Kongamano la biashara na uwekezaji, Dar es Salaam .


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa wameshiriki kama Wageni Rasmi kwenye kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Kongamano hilo limefanyika tarehe 15 Agosti, 2019 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam sambamba na Mkutano wa Wakuu wa Nchini wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)


Katika hotuba yake, Mhe Dkt. Magufuli amesema kwamba Afrika Kusini imepiga hatua katika maendeleo, technolojia na mitaji. Hivyo amewakaribisha kuja kuwekeza Tanzania kwenye kuongeza thamani madini, mazao ya kilimo (pamba), uvuvi, ufugaji (nyama na ngozi), uzalishaji wa mafuta ya kula, sukari, uunganishaji wa magari, uzalishaji wa madawa na vifaa tiba. Lengo ni kuiwezesha nchi kufikia hatua kubwa ya kusafirisha nje bidhaa zilizoongezewa thamani ili kukuza uchumi wa Taifa.


Vilevile, Mhe. Magufuli amefafanua na kuwahakikishia wafanyabiashara/wawekezaji wa pande zote mbili namna ambavyo Serikali inavyoendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hususani uwekwaji na uimarishaji wa miundo mbinu. Jambo hili limewekewa mkazo ili kufungua zaidi fursa kwenye sekta mbalimbali na kuwezesha wafanyabiashara na wawekezaji kuanzisha miradi ya uwekezaji zaidi.


Naye Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe.Ramaphosa amesema kwamba Afrika Kusini itaendelea kufanya biashara na uwekezaji pamoja/baina ya Tanzania ili kuinua uchumi wa nchi zote mbili. Hivyo amehimizanchi zote kuendelea kupanga na kutekeleza mikakati ya kuondoa vikwazo katika maeneo ya biashara na uwekezaji ili kuongeza imani ya wafanyabiashara na wawekezaji kwa Serikali zao na pia kuamsha ari ya kuanzisha miradi zaidi.


Katika kongamano hilo Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe ametoa mada ya mazingira na fursa za uwekezaji,vivutio vinavyotolewa kwa wawekezaji  (wazawa na wageni). Vilevile Mwambe ameelezea namna ambavyo wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Tanzania wanavyosaidiwa na TIC kupitia mfumo wa mahala pamoja (One Stop Facilitaion Centre) kupata vibali, vyeti na leseni zote muhimu anazohitaji mwekezaji kuwa nazo ili kuanzisha mradi wake nchini.

 

Kwa pamoja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe.Cyril Ramaphosa wametoa wito kwa nchi wanachama wa SADC kushirikiana kwa kutumia fursa za pamoja zinazopatikana ndani ya Jumuiya yao katika nyanja za uchumi na biashara kwa manufaa ya nchi zote.

 

Kongamano pia limehudhuriwa na Mawaziri, Naibu Waziri, Wabunge, Wakuu wa Taasisi na Makampuni ya Sekta Binafsi, na Wafanyabiashara kutoka Tanzania Bara na Visiwani na Afrika Kusini.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)