The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Wawekezaji wa nchi ya Uingereza waliowekeza nchini wamezungumza na Serikali kupitia Mdahalo wa Uwekezaji .


June 2019: Kuboresha mazingira ya uwekezaji ni mkakati endelevu wa Serikali ili kuwezesha wawekezaji waliopo nchini kufanya uwekezaji wao kwenye mazingira rafiki na pia itasaidia kuvutia wawekezaji wapya. Hayo yamezungumzwa Mei 29, 2019, katika ukumbi wa mikutano wa Coral Beach Hoteli, Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ushiriki wake kama mgeni rasmi kwenye mdahalo wa uwekezaji kati ya Serikali na wawekezaji wa Uingereza waliowekeza nchini. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde pia ameshiriki mdahalo.

Mdahalo huo ni wa pili kufuatia wa China uliofanyika mwezi Aprili, 2019. Lengo ni kuwezesha wawekezaji kuwasilisha kwa Serikali moja kwa moja kero/changamoto wanazokumbana nazo na pengine kukwamisha utekelezaji wa majukumu yao nchini. Vilevile kupitia mdahalo huo wawekezaji wamepokea majibu/ufafanuzi wa masuala waliyowasilisha hivyo kuongeza imani kwa Serikali. Aidha, kupitia mdahalo huo, pia Serikali imepokea maoni/ushauri kutoka kwa wawekezaji/wafanyabiashara namna ambavyo inaweza kutekeleza masuala mbalimbali yanayogusa biashara / uwekezaji wao wakati wakilinda wawekezaji walipo na pia ikidhamiria kuvutia wawekezaji wapya.

‘Serikali itaendelea kutafuta suluhu kwa changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara kuzingatia mchango na umuhimu wa sekta binafsi ambayo ndiyo mhimili mkuu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu’ amesisitiza Waziri Kairuki.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. Sarah Cooke ameipongeza Serikali kufanikisha mdahalo huo na ameuchukulia kama njia bora ya Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za uwekezaji. Aidha Mhe. Balozi amesema kuwa mdahalo umetoa majibu ya masuala mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza kwa wawekezaji wa Uingereza katika kutekeleza uwekezaji wao nchini. Ameyataja baadhi ya masuala hayo ni ukosefu wa ardhi ya uwekezaji iliyo tayari ‘landbank’, ugumu katika kupata vibali vinavyotakiwa kwa ajili ya uwekezaji, urasimu katika kupata idhini mbalimbali za kufanikisha uwekezaji na kuwapo kwa kaguzi na tozo nyingi kutoka kwa mamlaka tofauti za Serikali.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kupitia Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji Bw. John Mnali ametumia mdahalo huo kuipongeza nchi ya Uingereza kuwa nchi ya pili kati ya nchi kumi zilizowekeza nchini. Kwa kuzingatia hilo, amewakaribisha zaidi wawekezaji kutoka Uingereza kuendelea kuwekeza nchini kwa kupanua uwekezaji wao uliopo ama kuanzisha uwekezaji mpya kwenye maeneo ya sasa ya serikali ya kipaumbele ambayo ni uanzishaji wa viwanda, kilimo na uongezaji thamani, madini na uongezaji thamani, uvuvi na uongezaji thamani, madawa na vifaa tiba na uunganishaji wa magari. TIC imewahakikishia wawekezaji wa Uingereza utayari wake wa kuwasaidia ili kufanikisha zaidi uwekezaji wao nchini.

Kiujumla, mdahalo ulikuwa shirikishi kati ya Serikali na sekta binafsi hususan wawekezaji/wafanyabiashara kutoka nchini Uingereza ambapo wamepata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao na kutolewa majibu/ufafanuzi na Mawaziri/Naibu Waziri/Wakuu wa Taasisi/ Viongozi /Wataalamu na Wawakilishi wa Taasisi za Serikali. Wizara/Taasisi/Idara hizo ni PMO, TIC, TNBC, TRA, Uhamiaji, Kazi, Ardhi, NEMC, TBS, TFDA, OSHA, EPZA na BRELLA. Sekta binafsi pia iliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw.Godffrey Simbeye.

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)