The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE‘Hongera sana Wanawake wa TIC, nyie ni chachu ya mafanikio ya Kituo. .


‘Hongera sana Wanawake wa TIC, nyie ni chachu ya mafanikio ya Kituo. Mjiamini, mjiendeleze na   muwajibike ipasavyo ili kuleta tija kwa taasisi yetu na Taifa kwa ujumla’ Mkurugenzi Mtendaji wa TIC,  Mwambe

 

 Leo tarehe 8 Machi, 2019, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeungana na Wanawake wote nchini kusheherekea siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi. Sherehe hizo ambazo zimefanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam zimeshirikisha Wanawake kutoka pande mbalimbali za nchi. Mgeni rasmi alikuwa ni Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kauli mbiu ya mwaka huu ilikua ‘Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu’.

 

 Katika kufanikisha tukio hilo  muhimu, sherehe  zilipambwa kwa maandamano, maonesho na utoaji wa elimu kwa Wanawake kupitia hotuba ya Mgeni Rasmi na Viongozi mbalimbali walioshiriki pamoja na mada zilizowasilishwa kuhusu mifuko ya uwezeshaji, utaratibu wa kupata mikopo Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu na fursa mbalimbali za kiuchumi.

 

Kupitia maadhimisho ya sherehe hizo ni wazi kwamba Wanawake wamebaini fursa mbalimbali  za uchumi na TIC kama mdau wa masuala ya uwekezaji inawahamasisha Wanawake wote  kuchangamkia  fursa za uwezeshaji zinazotolewa na taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kuwekeza katika fursa mbalimbali za uchumi nchini kwa maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla.

 

Kipekee kabisa Mkurugenzi Mtendaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe katika siku hii muhimu ametoa hamasa kwa watumishi Wanawake wa TIC ambapo amewakumbusha kutambua kuwa wao ni mhimili wa Kituo katika kutekeleza majukumu yake hususan kuwahudumia wawekezaji katika kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli yanayolenga kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025. 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)