The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Kampuni ya Elsewedy imeichagua Tanzania kama nchi bora kwa kujenga kiwanda cha kuzalisha vifaa vya umeme kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. .


Miezi sita tangu kuapishwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Kazi amefanikisha kutekelezeka kwa majukumu kadhaa ikiwemo kuanza kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha vifaa vya umeme cha Elsewedy Cables kutoka nchini Misri. Mradi huu mkubwa wa utengenezaji wa vifaa vya umeme unatarajia kuwekeza zaidi ya Tsh. bilioni 100 na utazalisha transfoma, mita za umeme, nyanya za umeme na ‘cable’ kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya umeme. Kuanza kwa mradi huu ni hatua kubwa baada ya uwepo wa ucheleweshwaji wa upatikanaji wa ardhi. Hayo yamejiri hivi karibuni wakatiDkt. Kazi pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka walipofanya ziara ya pamoja kwenye kiwanda cha kampuni hiyo Wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.

 

Kiwanda hicho kimepata eneo lenye ukubwa wa Kilomita za Mraba 120,000 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha nyaya za umeme tani 15,000 kwa mwezi, Mashine za kupozea umeme (transfoma) 400 kwa mwezi na bidhaa nyingine muhimu zinazohitajika kwenye uzalishaji wa umeme katika viwango vya Kimataifa.

 

Akizungumzia kwa undani kuhusiana na ujio wa kiwanda hicho, Mkurugenzi wa kampuni ya Elsewedy Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Ibrahim Qamar amesema, kwa muda mrefu walikuwa na nia ya kujenga kiwanda kikubwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati lakini hawakufahamu ni nchi gani wanaweza kujenga. Walichukua hatua ya kufanya utafiti wa kina kwenye nchi mbabalimbali juu ya masuala waliyokuwa wanatamani kuyapata  ili kufanya maamuzi ya kujenga kiwanda hicho. Hatimaye wakabaini na kuafiki kwamba kwa aina ya mradi wao, Tanzania ni nchi bora zaidi kwa uwekezaji huo.

 

Bw. Qamar ameyataja baadhi ya mambo yaliyowavutia hadi kufanya maamuzi ya kuleta mradi huo mkubwa Tanzania ni pamoja na uwepo wa amani, utulivu, sera nzuri za uwekezaji chini ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, uwepo wa masoko ya ndani na nje ya nchi, sambamba na miundombinu itakayowawezesha kusafirisha kwa urahisi maligahfi na bidhaa ndani na kwenye nchi nyingine za Afrika na hata Ulaya.

 

Aidha Bw. Qamar pia ameeleza kufurahishwa kwake na uwepo wa TIC na huduma wanazotoa kwa wawekezaji ambazo na wao pia wamenufaika nazo. ‘Uwepo wa TIC umerahisisha safari na mchakato wa mradi wetu kukamilika na hatimaye kuanza. Aidha tunampongeza Mkurugenzi Dkt. Kazi na timu yake kwa jitihada walizochukua  kuishawishi Bodi ya kampuni ya Elsewedy kuichagua Tanzania kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa vifaa vya umeme kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Akihitimisha Bw. Ibrahim amesema kiwanda hicho mbali na kuzazilsha bidhaa zake kwa mfumo wa technolojia ya kisasa ikiwemo utumiaji wa roboti, kitatoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 400.Kiwanda hicho pia ili kuwa na wataalam kulingana na mahitaji yao, kimejipanga kujenga Chuo cha Ufundi (umeme) kwa ajili ya kuwanoa wafanyakazi watakaoajiliwa kiwandani hapo kila mara. Lengo la kiwanda hicho ni kuzalisha bidhaa bora zaidi za kisasa zitakazoitangaza Tanzania Kimataifa zaidi kupitia sekta ya nishati.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa (TIC), Dkt. Maduhu Kazi amewashukuru wawekezaji hao kwa kuichagua Tanzania kama nchi bora kwa uwekezaji wao na amewahakikishia ushirikiano wa hali ya juu kutoka kila Taasisi wezeshi katika kuhakikisha kwamba mradi huo unatekeleza majukumu yake kwa wakati na kufikia malengo yake ikiwemo kuanza uzalishaji ifikapo Juni 2021.

 

‘Hitaji la Serikali ni kupata miradi mikubwa na yenye tija kwa Taifa, hivyo hakutakuwa na sababu za uwepo wa ucheleweshwaji huduma yeyote kwa uwekezaji huu’, amesema Dkt. Maduhu.

 

Akielezea, Dkt. Kazi amesema kwamba, kuanza kwa mradi huo kutakuwa na manufaa mengi ikiwemo uzalishaji wa bidhaa nyingi ambazo awali zilikuwa zikinunuliwa nje ya nchi na kuigharimu nchi mabilioni ya fedha, kuzalisha bidhaa za ziada ambazo zitauzwa nje ya nchi kwenye nchi mbalimbali  na kuiingiza nchi fedha za kigeni,kuitangaza nchi Kimataifa pamoja na  kuleta tekonolojia ya kisasa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO  Dkt. Tito Mwinuka amebainisha kuwa uwekezaji huo ambao utajikita katika uzalishaji wa vifaa vya umeme,utarahisisha na  utafanikisha miradi mbalimbali ya umeme inayoendelea nchini kwa haraka kwa kuwa vifaa vitakuwa vikipatikana nchini tena kwa gharama nafuu. Hii ni kutokana na kuondokana na tegemeo la kupata vifaa husika nje ya nchi jambo ambalo wakati mwingine limekuwa likichukua muda mrefu kutoka kuagiza hadi kufika kwake, amesema Dkt. Mwinuka.

 

Dkt Mwinuka amehitimisha kwa kusema, kiujumla tunatarajia ujio wa mradi huo utawezesha kasi ya TANESCO kuongezeka katika kufanikisha miradi ya umeme nchini kwa kuwa bidhaa zinazohitajika katika kuunganisha na kusambaza umeme zitakuwa zikipatikana kwa wakati. Pia Dkt mwinuka amesisitiza kwamba shirika litaendeleza Sera ya nchi ya kutumia vifaa vinavyozalishwa ndani ya nchi hivyo kuwapa uhakikia wa soko la bidhaa zitakazozalishwa na kampuni hiyo.

 

Kampuni ya Elsewedy ina viwanda 25 katika nchi mbalimbali za Afrika na Afrika ya Kati,na kutokana na ubora wa bidhaa zake, kampuni ina masoko ya uhakika kwenye nchi nyingi duniani.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)