The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Jamii yafurahia faida za uwekezaji wa moja kwa moja kufuatia mwekezaji kuwakabidhiwa miradi ya Elimu .


Mwekezaji wa Kiwanda cha kuchakata Pamba cha Alliance Ginnery cha Mkoani Simiyu ameikabidhi Serikali Shule ya Sekondari Salama Bugatu iliyopo Wilayani Magu, Mkoani Mwanza na Chuo cha Ufundi Kasoli kilichopo Mkoani Simiyu. Miradi hiyo ya Elimu imekabidhiwa kwa kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambao ndio wenye Mamlaka ya kusimamia Uwekezaji nchini ambapo mradi wa Mwekezaji huyo umesajiliwa na TIC.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Dkt.Maduhu Kazi ndiye aliyepokea miradi hiyo kwa niaba ya Serikali ambapo amesema TIC inatambua mchango mkubwa unaoletwa na wawekezaji kwa nchi na jamii kwa ujumla, hivyo Serikali itaendelea kuvutia na kufanikisha uwekezaji nchini. Dkt. Kazi aidha amesema, TIC inasisitiza sana suala la wawekezaji kuwafikia wananchi wanaowazunguka kwa kuwapelekea miradi yenye manufaa ili waweze kufaidika na matunda ya uwekezaji hatua ambayo pia inasaidia kuboresha mahusiano kati ya Wawekezaji na jamii husika. 

 

"Nawapongeza wawekezaji kwa hatua ya kurudisha fadhila kwa wananchi kwa kuwajengea Shule na Chuo kwa  maendeleo ya jamii, tutazidi kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zitakazoibuka kwa lengo la kukwamisha uwekezaji nchini" amesema Dkt. Kazi

 

Naye Meneja wa kiwanda cha Alliance Ginnery Bw. Boaz Ogola wakati akikabidhi Shule na Chuo amesema, lengo la kuamua kujenga Shule na Chuo ni kutokana na kuwepo kwa umbali mrefu wa wanafunzi pamoja na kukosekana kwa fursa ya kujiendeleza kielimu kwa wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu. Uwepo cha Chuo cha Ufundi kitawawezesha kupata stadi za kujiajiri wenyewe ikiwemo ufundi wa kushona.

 

"Ujenzi wa Shule ya Sekondari umegharimu Tsh. milioni 150 na Chuo cha Ufundi umegharimu Tsh.milioni 180, tuliona ni muhimu kujenga Shule ili kuwapunguzia umbali na pia tuliamua kujenga chuo baada ya kubaini wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wanakosa fursa ya kujiendeleza ikiwamo elimu ya ufundi itakayowawezesha kujiajiri" alisema Bw. Ogola.

 

Aidha Bw. Ogola alibainisha kuwa bado wanaendelea kukamilisha mpango wao wa kujenga darasa litakalotumika kama karakana ya wakulima ili kuwajengea uwezo wananchi kuwa na Kilimo cha kisasa cha kibiashara na hatimaye kuwaepusha na kilimo cha mazoea ambacho hakina tija.

 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Antony Mtaka wakati akipokea Chuo cha Ufundi ameziagiza Mamlaka zinazohusika kuanza mara moja kisajili Wanafunzi wanaomaliza darasa la saba.

 

Kuhusu Karakana itakayojengwa Mhe. Mtaka amewahakikishia Wananchi  kuwa itakuwa ni fursa nzuri ya kujifunza kilimo bora cha pamba na chakula ikiwepo unenepeshaji wa mifugo na ufugaji wa kuku.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Bw. Kali amemshukuru mwekezaji kwa msaada huo na kubainisha kuwa umesaidia kutatua changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

 

Nao Wananchi kwa pamoja wamefurahia ujio na uwepo wa uwekezaji huo kwa kuwa tayari manufaa ya miradi ya aina hiyo inaonekana na yanawafikia moja kwa moja kupitia ajira, malighafi, kipato, elimu, ufundi na maendeleo kiujumla. Wametoa wito kwa wawekezaji wote nchini kuangalia namna bora ya kutekeleza na kuendesha miradi yao ya uwekezaji na  wakati huo  wakileta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi  wanaowazunguka kupitia miradi ya kiuchumi na jijamii.

 

Pongezi kwa Meneja wa TIC Kanda ya Ziwa  Bi. Pendo Gondwe kuratibu na kuhakisha mradi huo unapata huduma  stahiki ili kuanza utekelezaji.

 

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)