The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Benki ya Maendeleo ya Afrika Kunufaisha Wawekezaji Nchini Kupitia Serikali, Benki na Pia Mtu Mmoja Mmoja .


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt.Maduhu Kazi amesema ipo haja Kwa wawekezaji nchini hususan wazawa, kuitumia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa mikopo ili kukuza mitaji yao. Ameyasema hayo katika kikao cha pamoja cha Mkurugenzi huyo wa TIC, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini Tanzania (AfDB) Dkt.Alex Mubiru na Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Bw.Paul Koyi kilichofanyika katika ofisi ya TIC Jijini Dar es Salaam ambacho kilijadili namna ya kuendelea kifanikisha Uwekezaji nchini.

 

Dkt. Kazi amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya jitihada nyingi za kuboresha mazingira ya uwekezaji lengo likiwa ni kuvutia uwekezaji zaidi jitihada ambazo zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuifanya Tanzania kupaa kiuchumi. Amezitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya kuchakata na kutoa vibali na leseni mbalimbali pamoja na kuondoa kodi ambazo zilionekana kuwa mzigo kwa Wawekezaji.

 

*"Uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB nchini ni hatua nzuri katika kufanikisha miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali"* amesema Dkt. Kazi.

 

Amesema huduma za Benki ya AfDB ni muhimu hususan kwa Wawekezaji wanaokabiliwa na changamoto za mitaji na kuwahimiza watanzania kuchangamkia fursa za mikopo katika Benki hiyo ambapo pia aliipongeza Serikali kwa kudumisha uhusiano na Benki hiyo ambayo yamefanikisha Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo.

 

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB Tanzania Dkt. Mubiru amesema Benki hiyo itaendelea kuisaidia na kushirikiana na Serikali pamoja na Sekta Binafsi katika kufanikisha shughuli za kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa kwa kutoa fedha ambazo ni mkopo au msaada.

 

Amesema, fedha zinazotolewa na AfDB kwa shughuli za maendeleo nchini zinawafikia wananchi kwa njia mbalimbali kupitia Serikali pale inapotekeleza shughuli za maendeleo; kupitia mabenki au mashirika kwa watu yenye uhitaji wa fedha za kufanikisha  miradi midogo na ya kati na kwa mtu mmoja mmoja mwenye miradi mikubwa yenye thamani ya kuanzia Dola za Kimarekani Milioni 30$.

 

Alibainisha miradi yenye ushawishi mkubwa na yenye nafasi ya kunufaika na fedha za AfDB ni ile inayaojikita katika uwekezaji wa kwenye maeneo ya mnyororo wa thamani, teknolojia nchini, kilimo cha mazao yanayotumika na viwanda vya ndani na nje na yale yanayoagizwa zaidi kutoka nje ya nchi, kuongeza na kuendeleza uzalishaji ‘productivity’, wa mazao ya chakula na biashara mfano kilimo cha mhogo na ngano na kuwaasa Wananchi kuanzisha miradi ya uwekezaji katika maeneo yenye ushawishi.

 

Akiwakilisha sekta Binafsi, Bw. Koyi amesema Sekta binafsi kwa sasa inaendesha biashara na uwekezaji wake katika mazingira ya uwazi na kuongeza kuwa jitihada hizo ni matokeo ya maboresho yanayofanywa na Serikali kila mara jambo ambalo linahamasisha sekta binafsi.

 

"Kwa mazingira yaliyopo, kwa sasa sekta binafsi imehamasika kwa kiasi kikubwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya biashara/uwekezaji" amesema Koyi.

 

Aidha, Bw. Koyi amemkaribisha Dkt. Mubiru kuongeza mwanya wa kushirikiana na Wadau wa Sekta Binafsi  kupitia makongamano na mikutano ya pamoja yenye mlengo wa kutoa elimu kwa wananchama ili kufahamu kwa undani wa Shirika la AfDB. Pia elimu inaweza kujikita katika kuainisha kazi za AfDB, miradi/sekta zinazosaidiwa na AfDB na vigezo vya kupata fedha hizo.

 

 Hatua hiyo ni muhimu kuwezesha wananchama/wananchi wengi kupata uelewa wa namna ya kunufaika na fursa/bidhaa zinazotolewa na AfDB nchini. Suala hilo lilikubaliwa na Mkurugenzi wa AfDB na mikakati ya kufanikisha itafuata ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mtaji wa kufanikisha biashara na uwekezaji nchini.

 

 

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)