The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kanda ya Kaskazini kimeendesha mafunzo ya biashara/ uwekezaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) .


Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kanda ya Kaskazini kimeendesha mafunzo  ya biashara/ uwekezaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) kwa Kanda ya Kaskazini kwenye Wilaya ya  Korogwe (Tanga) na Mwanga (Kilimanjaro). Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wajasiriamali katika masuala mbalimbali ya uwekezaji na biashara na pia kuibua fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wajasiriamali na wawekezaji wa ndani katika Kanda hiyo.

 

Mafunzo hayo yamesaidia wajasiriamali kujua namna TIC inavyoweza kuwasaidia wawekezaji kupata leseni na vibali mbalimbali kupitia mfumo wa Huduma za Mahali Pamoja, na pia namna  ambavyo Wajasiriamali wanavyoweza kuunganishwa na wawekezaji wakubwa ili kujipatia fursa za kusambaza huduma/ malighafi, kupata masoko,  ajira na kipato.

 

Kwa Wilaya ya Mwanga, mafunzo yamefunguliwa 1 Septemba, 2020 na Mkuu wa Wilaya Mhe. Thomas Apson Mwang'onda, ambaye amekishukuru Kituo kwa jitihada zake za kusaidia wajasiriamali katika kushiriki kwenye masuala ya uwekezaji. Aidha kwa kuzingatia kwamba changamoto kubwa kwa wajasiriamali Wadogo na wa Kati ni ukosefu wa mitaji, Mhe. Mwang'onda ameshauri taasisi za fedha kuwawezesha kifedha wajasiriamali kote nchini kwa masharti nafuu kuliko inavyofanyika hivi sasa ili waweze kutekeleza miradi ya uwekezaji na biashara kwa manufaa ya nchi yetu.

 

Katika mafunzo hayo, TIC imeweza kushirikiana na wadau wengine kama Taasisi za Fedha (NMB, CRDB, AZANIA, KCB), Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), NSSF, TRA, VETA, SIDO na TCCIA.

 

Jumla ya washiriki wapatao 72 wameshiriki mafunzo hayo katika Wilayani Mwanga na washiriki takribani 65 katika Wilaya ya Korogwe. Wilaya zote zinakaribisha wawekezaji wa ndani na wa nje ya nchi kwa kuwa tayari maeneo kadhaa ya ardhi kwa ajili ya kuvutia uwekezaji yametengwa.

 

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)