The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Kampuni ya Scania imeona fursa ya kuzalisha mabasi ya abiria yanayotumika mijini.Waziri awashukuru kwa imani walioionyesha kwa Tanzania .


Kufuatia fursa za uwekezaji zilizopo nchini kama zilivyowasilishwa na  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanznaia (TIC) Geoffrey Mwambe katika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi ya Sweden tarehe 12 Machi,2020, Dar es Salaam  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Scania Bw. Lars Eklund amefika na kufanya mazungumzo na Mhe. Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kwa lengo la kujadili zaidi azma ya Kampuni ya Scania hiyo kufanya uwekezaji mkubwa hapa nchini kwa kujenga Kiwanda cha kuunganisha mabasi. 

 

Kampuni ya Scania ni wazalishaji wakubwa wa malori ya mizigo pamoja na magari makubwa ya kisasa ya abiria (mabasi) yanayotumika katika usafiri wa mijini na hubeba abiria wengi kwa wakati mmoja. Aidha imeelezwa kwamba mabasi hayo pia yana uwezo wa kutumia mafuta (dizeli) au gesi ya CNG kadiri mteja atakavyohitaji. Mabasi ya Kampuni hiyo yanayotumia CNG yanasifika kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji. Kwa sasa Scania ina uwezo wa kutengeneza Mabasi ya aina hiyo yanayotumia nishati yenye viwango vinavyokubalika kimataifa vya Euro 5 na Euro 6.

 

Katika kikao, Bw. Eklund amemweleza Mheshimiwa Waziri kuwa wamevutiwa kuanzisha Kiwanda hicho hapa nchini kwa kuzingatia mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwamo upatikanaji wa wingi wa gesi asilia ambayo ni rasilimali muhimu katika uendeshaji wa Mabasi yanayotumia nishati ya CNG. Aidha, alieleza pia kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa Mabasi yenye uwezo mkubwa wa kusafirisha abiria mijini katika nchi za Afrika Mashariki na kwamba wanatarajia pia uhitaji huo utazidi kuongezeka hadi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Kwa upande wake Waziri Kairuki amemkaribisha mwekezaji huyo na kumhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kuukaribisha uwekezaji huo wa Scania. Amemsihi pindi watakapokamilisha taratibu zao na kufikia uamuzi wa kuanza kujenga Kiwanda hicho mradi upitie Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kurahususha na kuwezesha mradi kuanza na kukamilika kwa wakati.

 

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Kairuki amemshukuru Bw. Eklund kwa imani waliyoionesha kwa Tanzania hadi kufikiria kuanzisha mradi huo hapa nchini.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC amewasilisha na kufafanua mada ya mazingira ya uwekezaji, hali ya uchumi, sababu za kuwekeza Tanzania, fursa za uwekezaji, vivutio vya uwekezaji  na umuhimu wa kusajili miradi ya uwekezaji  naTIC. Sweden ni moja ya Nchi zenye makampuni yaliyowekeza hapa nchini ambapo jumla ya makampuni 113 yamewekeza hapa nchini yenye mitaji thamani ya Dola za Marekani 834.42 na kutoa ajira za moja kwa moja kwa Tanzania 3,981.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)