The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Uchumi wa Tanzania umetabiriwa kuendelea kupaa katika kipindi kifupi kijacho, taarifa ya Wataalam wa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) Machi,2020. .


Jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kusimamia madhubuti utekelezaji wa Sera za fedha na uchumi hususan kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, pamoja na usimamizi wa Benki, zimeelezwa kuwa ni miongoni mwa vitu vinavyoianya uchumi wa Tanzania kukua na kuendelea kukua kwa kasi katika siku zijazo.

 

Kwa mujibu wa ripoti ndogo iliyotolewa Jijini Dar es Salaam na wataalam wa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) zimeeleza kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zinazofanya vizuri katika ukuaji wa Uchumi. Utafiti huo umefanyika kuanzia tarehe 20 Februari hadi Machi 4, 2020.

 

Kiongozi wa timu ya IMF iliyotembelea Tanzania Enrique Gelbard  amesema kiwango cha ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miezi michache iliyopita kinaonyesha ukuaji wa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali, kuongezeka kwa mauzo ya nje ya nchi, pamoja na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi.

 

Amesema viashiria hivyo vitaifanya Tanzania kuendelea kukua kiuchumi katika siku zijazo katika sekta za ujenzi na madini, unaosaidiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei kwa kiwango cha asilimia 3.7 pamoja na kuimarika kwa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni,kadhalika na uwepo wa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni inayoweza kufanya manunuzi kwa kipindi cha takribani miezi mitano.

 

Aidha mtaalam huyo amezungumzia kuimarika kwa uchumi hapa nchini kuwa kumesababishwa na sera madhubuti za usimamizi wa fedha ambazo zimeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi hapa nchini, pia amezipongeza mamlaka husika kwa kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato.

 

Taarifa ya IMF inaielezea Tanzania kuwa nchi/sehemu bora kwa wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali. Hii ni kutokana na kuwapo kwa uchumi imara sambamba na mazingira bora ya uwekezaji (uwepo wa ardhi, watu, nishati, masoko na sera bora). Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye miradi ya viwanda, kilimo, uzalishaji wa mafuta ya kula, uzalishaji wa sukari, uongezaji thamani mazao ya uvuvi, uunganishaji wa magari, uzalishaji wa madawa na vifaa tiba, ujenzi wa hospitali na utalii.

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)